Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez
akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Anne Rose Nyamubi mara
baada ya kuwasili ofisini kwake kwa ajili ya mazungumzo kabla ya
kuelekea kwenye kituo cha kulelea watoto wenye mahitaji maalum wakiwemo
walemavu wa ngozi cha Buhangija Jumuishi kilichopo mkoani Shinyanga.
Na mwandishi wetu, Shinyanga
MKUU wa wilaya ya Shinyanga AnneRose Nyamubi ameomba jamii ya
watanzania kusaidia kupatikana kwa zahanati katika kituo cha kulelea
watoto walemavu cha Buhangija ili kupunguza adha wanazopata watoto hao
katika huduma za afya.
Kauli hiyo ameitoa katika mazungumzo na mwandishi wa habari hizi
ambaye alifika katika kituo hicho akiambatana na ujumbe wa Umoja wa
Mataifa uliokuwa ukiongozwa na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa
Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP)
nchini, Alvaro Rodriguez.
Nyamubi amesema kwamba ingawa hospitali ya mkoa ina dirisha kwa ajili
ya matibabu ya watoto hao,wakati mwingine inakuwa shida daktari maalumu
anayehusika anapokuwa hayupo.
Aidha alisema kwa namna watoto hao walivyo wanahitaji huduma ya
karibu ya kitiba ambayo inawezekana kama kituo hicho kingekuwa na
zahanati yake.