Tuesday, December 23, 2014


MBUNGE wa Sengerema (CCM), William Ngeleja ameweka wazi kuwa pamoja na ushindani kuwa mkubwa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni, anajivunia ushindi mzito walioupata kupitia chama chake.

Uchaguzi huo ulifanyika nchi nzima Desemba 14, mwaka huu ambapo licha ya kasoro ndogondogo zilizojitokeza katika baadhi ya maeneo na kusababisha kurudiwa kwa mara ya pili, Desemba 21, CCM imeonesha kufanya vizuri katika maeneo mengi.
Akizungumza na mwanahabari wetu, Ngeleja alisema anafahamu namna ambavyo upinzani ulikuwa umejipanga kuhakikisha wanashinda lakini hakuna jinsi inabidi wakubaliane na matokeo kwamba chama chake kimeibuka kidedea katika jimbo lake.
“Katika jimbo langu la Sengerema, kwa vijini CCM tumepata ushindi wa asilimia 85 wapinzani wakiambulia 15, vilevile katika vitongoji, CCM tumepata asilimia 82 wao wamepata 18 hivyo hiyo ni ishara tosha kwamba tunakubalika.
“Niwaahidi tu wakazi wa Sengerema kwamba hatutabweteka katika kazi ambayo wametupa kuisimamia. Ilani yetu ni kuhakikisha tunaleta maendeleo ya kila mwananchi wa jimbo letu na hata taifa kwa jumla,” alisema Ngeleja.
Ngeleja alisema ana imani kabisa ushindi wa CCM hauishii katika ngazi hiyo pekee bali hata ngazi za madiwani na wabunge hivyo wanaahidi kusimamia ilani na ahadi ambazo walizitoa kwa wananchi wanazitekeleza.
Uchaguzi huo uliofanikiwa kwa kiasi kikubwa, ulisimamiwa  na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

0 comments:

Post a Comment

Design by hons.CISKO | Blogger Theme by CISKO